SERENGETI BOYS YAIKOSAKOSA AMAJIMBOS
TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa
miaka 17, Serengeti Boys imelazimishwa sare ya bila kufungana na Afrika Kusini,
Amajimbos katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Pili kuwania tiketi ya kucheza
Fainali za Afrika, uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanamaanisha, Serengeti Boys
itahitaji sare ya mabao katika mchezo wa ugenini, au kushinda kabisa ili
kuingia hatua ya mwisho ya mchujo katika kuwania tiketi ya Fainali zitakazopigwa
Niger mwakani.
Amajimbos waliuanza mchezo vizuri wakilitia
kwenye misukosuko lango la Serengeti kwa dakika takriban 20 za mwanzo, lakini
taratibu mchezo ulianza kubadilika na wenyeji wakageuza kibao.
Serengeti ilipoteza nafasi mbili za wazi za
kufunga kipindi cha kwanza na nafasi nyingine mbili zaidi za wazi pia za
kufunga kipindi cha pili, ambacho watoto wa nyumbani walitawala zaidi
mchezo.
Kocha wa Serengeti, Hababuu Ali alisema
kwamba vijana wake waliuanza mchezo kwa kuelemewa kutokana na woga wa kucheza
mbele ya umati wa mashabiki kwa mara ya kwanza lakini walipozoea waliendelea
vizuri.
Hababuu ameongeza kuwa Amajimbos si wazuri
kiufundi zaidi wana nguvu na kasi na kwa sababu hiyo ana matumaini ya kupata
matokeo mazuri ugenini.
Kikosi cha Serengeti Boys; Mitacha Mnacha,
Abdallah Jumanne/Mashaka Ngujiro dk23, Issa Baky, Adolph Mutasingwa/Kelvin
Farrel dk10, Martin Kiggi, Omar Wayne, Athanas Mdam, Ali Mabuyu, Abdul
Bitebo/Mohamed Mussa dk86, Prosper Mushi na Baraka Yussuf.
Amajimbos; Mondili Mpoto, Nelson Maluleke,
Simon Nqoi, Notha Ngcobo, Keanu Cupido, Tendo Mukumela, Katlego Mohamme,
Athenkosi Dlala, Sibongankonke Mbatha/Felix Noge, Luvuyo Mkatshana/Vuyo Mantjie
na Khanyiso Nayo.
Waooo thanks for the news
ReplyDelete